Rais Jakaya Kikwete amesema mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa na kuiwajibisha Serikali.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo
uboreshwe zaidi na uweze kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo, ni lazima
uendeshwe kwa watu kufuata sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya nguvu,
ambayo yanaweza kuvuruga nchi.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi na Usalama, aliyasema hayo juzi wakati alipotoa Mhadhara kuhusu
Usalama wa Taifa kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Kunduchi, jijini Dar es
Salaam.
Alikuwa anajibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili
kwenye chuo hicho kutoka Kenya, ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya
siasa, vinaathiri umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi
ya 30 ya Tanzania, kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika
na Waafrika.
Rais Kikwete alisema: “Vyama vingi ni vizuri. Mfumo
wa vyama vingi unaleta matumaini kwa kupanua wigo wa kisiasa, ambao haukuwa
mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa mtu anaweza kuamua kujiunga na chama chochote
cha siasa anachokipenda yeye.”
Aliongeza kusema: “Ni mfumo ambao unaiwajibisha
Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa demokrasia. Sasa watu wanaweza hata
kuamua kupunguza bajeti ya safari za Rais nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais
anaweza kufanikiwa zaidi na Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka zaidi kama
Rais atabakia amejifungia ndani ya nchi.”
Rais Kikwete alizidi kujibu swali hilo: “Jambo la
maana ni kwamba tunahitaji aina mbalimbali ya mawazo. Mawazo ya namna hiyo
hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo yanasaidia hata chama changu
kuimarika zaidi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema mfumo huo,
utavurugika, endapo baadhi ya watu wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja za
nguvu, badala ya kupambana kwa hoja na nguvu ya hoja.
“Wasiwasi wangu ni kuingiza matumizi ya nguvu katika
ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa watu kukimbilia kutumia nguvu baada ya
kushindwa kwenye hoja. Na hili halivumiliki na likitokea basi Serikali
itaingilia kati kudumisha amani,” alisema.
No comments:
Post a Comment