Na Hassan Hamad
(OMKR)
Mkutano Mkuu wa
CUF Taifa umemchagua tena Katibu Mkuu wa Chama hicho kuendelea na wadhifa huo
kwa kupata kura 675, sawa na asilimia 99.5 ya kura zilizopigwa.
Mkutano huo pia umemchagua Prof. Ibrahim
Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa kupata kura 659 sawa na asilimia 95.5
na kumshinda mpinzani wake Chifu Lutalosa Yemba aliyepata kura 30 sawa na
asilimia 4 nukta 3.
Aidha mkutano huo
umemchagua Mhe. Juma Duni Haji kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kupata
kura 662 sawa na asilimia 99.25.
Akizungumza baada
ya kutangazwa mshindi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad,
amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumpa tena ridhaa ya kuongoza chama
hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wakati wa
Kampeni, Mapema akizungumza katika kampeni za kuomba kuchaguliwa tena kuwa
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif amesema siri ya mafanikio yake kisiasa
ni kutokana na kujiamini kwake kuwa kiongozi, kuwa mkweli na kuwa na dhamira
njema kwa wananchi.
Akijibu hoja za
wajumbe wa mkutano huo Maalim Seif amewataka viongozi wa chama hicho
kutotangaza kuhudhuria kwa viongozi wa kitaifa kwenye mikutano ya hadhara hadi
pale wenyewe watakapothibitisha kuhudhuria, ili kuepusha wananchi kutoamini
utendaji wa viongozi hao.
Mgombea wa nafasi
ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Juma Duni Haji amesema iwapo
atachaguliwa kushika nafasi hiyo atashirikiana na viongozi wengine wa kitaifa
pamoja na wananchi kuhakikisha kuwa chama kinapata maendeleo zaidi.
Chifu Yemba
amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kutetea demokrasia ya kweli ndani ya chama
na taifa kwa ujumla. Chifu Yemba ambaye ni mwanasayansi kitaaluma, pia ni
Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Prof. Lipumba
amesema akichaguliwa atahakikisha anatembelea nchi nzima kuimarisha chama kabla
ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Aidha amesema atafanya juhudi za ziada kuona
kuwa Tanzania inakuwa na Muungano wa kuheshimiana baina ya pande mbili za
Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).
Amesema wanawake
watapewa nafasi ndani ya kamati tendaji ya chama kuondosha dhana ya mfumo dume
unaodaiwa kuwepo katika ngazi za juu za uongozi.
Mgombea mwengine
wa nasafi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa M’bezi Adam Bakar, amejitoa kwenye
kinyang’anyiro hicho na kubakia wagombea wawili wa nafasi ya Mwenyekiti.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliteuliwa kuwa
mwenyekiti wa muda wa kuongoza uchaguzi huo uliosimamiwa na mwanasheria Awadh Ali
Said.
Viongozi wakuu wa CUF wakionyesha mshikamano
baada ya kuchaguliwa kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wa pili kulia ni msimamizi wa uchaguzi huo Awadh Ali Said (Picha na Salmin
Said, OMKR)
Source:Michuzi
No comments:
Post a Comment