Thursday, June 26, 2014

SHINDANO LA REDD'S MISS SINZA 2014 KUFANYIKA KESHO MEEDA SINZA


Mratibu wa shindano la Redd's miss Sinza 2014 Tinna Matutuna katikati akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Meeda Night Club sinza juu ya Shindano la Redd's Miss Sinza litakalofanyika kesho ijumaa katika ukumbi wa Meeda Night Club kwa kiingilio cha 5,000 kwa viti vya kawaida na 10,000 kwa Viti Maalum .kushoto na kulia ni baadhi ya warembo wa shindano hilo.
=======  ====== =====
MNYANGE atakayefanikiwa kuibuka mrembo wa kitongoji cha Sinza ‘ Redds Miss Sinza  2014’ katika shindano litakalofamyika leo Ijumaa kwenye Ukumbi wa Meeda Night Club uliopo Sinza jijini Dar es Salaam atazawadiwa kitita cha Sh. 300,000.

 Akizungumza jana jijini, Mratibu wa shindano hilo, Tinna Makutika, alisema kuwa mshindi wa pili atajinyakulia Sh. 200,000, mshindi wa tatu  Sh. 100,000 huku warembo wengine waliobakia kila mmoja ataambulia zawadi ya kifuta jasho ya Sh. 50,000.

 Mratibu wa shindano hilo alisema kuwa maandalizi ya kinyang’anyiro hicho yamekamilika na anaamini Sinza mwaka huu itafanikiwa kutwaa taji la taifa ambalo linashikiliwa na mrembo kutoka Dodoma.

Alisema kuwa warembo wake wamejiandaa kuonyesha ushindani na kila mmoja amejipanga kufanya vizuri ili kushinda taji la Sinza usiku wa leo.
"Mwaka huu nina warembo wazuri na wenye vigezo vyote, naamini mwaka huu nitarudisha heshima ya watu wa Sinza ya  kufanikiwa kutoa mshindi wa taji la Redd's Miss Kinondoni  na Redd's Miss Tanzania mwaka 2014”, alisema Tinna.

Aliongeza kuwa wamejipanga kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Brigitte Alfred, ambaye alitwaa taji la taifa na kupata nafasi ya kuitangaza nchi kwenye mashindano ya dunia ya Miss World.Alisema pia shindano hilo linatarajiwa kuwa na burudani mbalimbali ikiwamo  bendi mahiri ya muziki wa dansi, FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ ambao wanatamba na Chuki ya Nini. Kiingilio cha juu katika shindano hilo ni Sh. 10,000 kwa viti maalum na vya kawaida ni Sh. 5,000.

Aliwataja warembo 12 watakaochuana ni Liliani Sandi,Priscar Sarakikya,Agnes Mwikombe,Esta Wilson,Rose Lucas,Zubeda Saburi,Tuku Harison,Dorine Benne,Farida Iddy,Qeenlatifa Hashim,Jane Masawe na Wahida Ahmed.

Naye Meneja wa kinywaji cha bia ya Redd’s Original, Victoria Kimaro, alisema ni muda muafaka kwa wapenzi wa tasnia ya urembo nchini wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria shindano hilo ili kushuhudia namna kitongoji cha Sinza kilivyo na bahati ya kutoa warembo wenye ushindani katika fainali za taifa.

Victoria alisema kuwa wadau wa sanaa ya urembo wanatakiwa kuona sanaa hiyo ni sehemu inayowapa nafasi wasichana kutimiza ndoto zao na hatimaye kujiendeleza kimaisha.

No comments:

Post a Comment