Uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia Kidato cha Tano katika
shule za Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2014 umekamilika. Uchaguzi
umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya watahiniwa waliofanya Mtihani
wa Kidato cha Nne Tanzania Bara mwaka 2013.
2.0 WATAHINIWA WALIOFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MWAKA
2013
Jumla ya watahiniwa 427,679 walisajiliwa kufanya Mtihani wa
Kidato cha Nne 2013, wakiwemo wasichana 199,123 sawa na asilimia 46.56 na
wavulana 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao watahiniwa 404,083 sawa na
asilimia 94.48 walifanya mtihani na watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52
hawakufanya mtihani huo.
2.1 Watahiniwa wa Shule (School Candidates)
Kwa Watahiniwa wa Shule, watahiniwa 367,163 walisajiliwa
kufanya mithanikati yao wavulana ni
198,099 na wasichana ni 169,064. ambapo watahiniwa 352,614 sawa na asilimia
96.04 walifanya mtihani; kati yao wasichana walikuwa 162,412 sawa na asilimia
96.07 na wavulana 190,202 sawa na asilimia 96.01. Watahiniwa14,549 sawa na
asilimia 3.96 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.
2.2 Watahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidates)
Kati ya watahiniwa 60,516 wa kujitegemea waliosajiliwa
kufanya mtihani, watahiniwa 51,469 sawa na asilimia 85.05 walifanya mtihani na
watahiniwa 9,047 sawa naasilimia 14.95 hawakufanya mtihani kwa sababu
mbalimbali.
Jumla ya watahiniwa 235,227 sawa na asilimia 58.21 ya
watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013 walifaulu. Mwaka 2012
watahiniwa waliofaulu walikuwa 185,940 kati ya 431,650 waliofanya mitihani; hii
ni sawa na asilimia 43.08. Matokeo haya yanaonesha kuwa mwaka 2013 ufaulu
umeongezeka kwa asilimia 15.13.
3.1 Ufaulu wa Watahiniwa wa Shule
Mwaka 2013 Watahiniwa wa Shule waliofaulu ni 201,152 sawa na
asilimia 57.05 ya watahiniwa 352,614 waliofanya mtihani. Kwa mwaka 2013 kuna
ongezeko la ufaulu wa watahiniwa 41,405, sawa na asilimia 25.91 ikilinganishwa
na ufaulu wa mwaka 2012 ambapo watahiniwa 159,747 walifaulu.
3.2 Ufaulu wa Watahiniwa wa Kujitegemea
Takwimu zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa
watahiniwa wa kujitegemea kutoka 26,193, sawa na asilimia 43.07 mwaka 2012 hadi
kufikia watahiniwa 34,075, sawa na asilimia 66.21 kwa mwaka 2013; Kwa
kulinganisha na mwaka 2012 lipo ongezeko la asilimia 30.09 kwa ufaulu wa
watahiniwa wa kujitegemea.
Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja
ya I -III umefikia watahiniwa 71,527 sawa na asilimia 20.28 ya watahiniwa
waliofanya mtihani Tanzania Bara.Hivyo kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia
106.73 ikilinganishwa na matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2012, kwa kuwa watahiniwa
wa shule waliofaulu katika madaraja I-III kwa mwaka huo walikuwa 34,599 sawa na
asilimia 9.67 ya watahiniwa waliofanya mtihani.
5.0TARATIBU ZA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO
2014.
Kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali, mwanafunzi
anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha tano na vyuo
vya Ufundi, hulazimika kujaza ‘Selform’ ambayo ndiyo fomu rasmi ya maombi. Kwa
kutumia fomu hiyo, mwanafunzi huchagua maombi matano ya tahasusi
(Combinations)za masomo anayotaka kusoma na shule anayotarajia kujiunga nayo
kwa kila chaguo.
Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi katika machaguo yake
ya masomo na shule kwa kuanzia na chaguo la kwanza. Kama mwanafunzi atakuwa
hana sifa katika machaguo yote aliyoomba, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la
somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi
kulingana na tahasusi na nafasi zilizopo katika shule husika.
6.0 IDADI YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA
TANO
Jumla ya Wanafunzi 54,085 sawa na asilimia 75.61 ya
wanafunzi 71,527 waliostahili kuingia Kidato cha Tano Tanzania Bara kwa mwaka
2014 wamechaguliwa; hilo ni ongezeko la wanafunzi 20,402 kwa kulinganisha na
wanafunzi 33,683 waliochaguliwa mwaka 2013. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa
2014 wavulana ni 31,352na wasichana ni 22,733.
Wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kidato cha Tano katika
jumla ya shule 241 zikiwemo shule 33 zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza
mwaka 2014.
Nawashukuru sana wadau wote wa elimu katika Halmashauri
mbalimbali kwa kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo maabara.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano 2014 ni
kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati yao wavulana 14,826 sawa
na asilimia27.41wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wavulana 16,526 sawa
na asilimia 30.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya Jamii.
Aidha,wasichana 7,859 sawa na asilimia 14.53wamechaguliwa kusoma masomo ya
sayansi na wasichana 14,874 sawa na asilimia 27.50 wamepangwa kusoma masomo ya
Sayansi ya Jamii.
Nawapongeza walimu wote kwa juhudi walizozifanya katika
ufundishaji kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji walizopata kupitia mpango wa
mafunzo kazini (INSET)kwa walimu wa sayansi na lugha (Kiswahili na Kiingereza)
unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi
ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa. Aidha nawapongeza
wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi.
Hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha vijana kusoma
masomo ya Sayansi zimeanza kuzaa matunda.
Natoa wito kwa wanafunzi wa jinsi zote kujisomea kwa bidii
masomo yote, yakiwemo ya Sayansi na Sayansi ya Jamii, kwani yanategemeana.
Walimu wa masomo ya Sayansi, Sayansi ya Jamii na Hisabati wanakumbushwa kutumia
mbinu shirikishi za kitaalam na kisaikolojia katika kufundisha ili kuwavutia
wanafunzi wengi zaidi kusoma na kufaulu mitihani yao. Aidha walimu wa masomo ya
Sayansi, waendelee kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi wakiwemo
wanafunzi wa kike. Aidha, wanafunzi wa kike wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza
masomo yote yakiwemo ya Sayansi, kwani siri ya kujifunza ni utayari.
7.0 WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI,
MWAKA 2014
Jumla ya wanafunzi 472wakiwemo wavulana 355 na wasichana 117
wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi. Idadiya wanafunzi hao imepungua
kutoka 530 mwaka 2013 hadi 472 mwaka 2014 kwa sababu kwa sasa vyuo hivyo
vimeanza kuchukua wanachuo wa shahada ya kwanza. Aidha, kutokana na ufaulu
kuongezeka idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo
imeongezeka kutoka wanafunzi 114 mwaka 2013 hadi wanafunzi 117mwaka 2014 sawa
na ongezeko la asilimia 2.63.
Natoa wito kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii masomo
ya sayansi ili mwakani idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi
iongezeke ili Taifa lipate wataalam wa kutosha wa ngazi zote.
8.0 SABABU ZA WANAFUNZI KUKOSA KUCHAGULIWA KUINGIA KIDATO
CHA TANO
Jumla ya wanafunzi 16,800 wakiwemo watahiniwa wa kujitegemea
10 waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo:
ufinyu wa nafasi za shule za Kidato cha Tano (wanafunzi 16,400) na kukosa
tahasusi - Combination (wanafunzi 400).
Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili baada
ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na wanafunzi ambao
hawakuripoti awamu ya kwanza. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia
nafasi ya kusoma kidato cha Tano na cha Sita kwa pamoja na shahada ya Ualimu
wanafunzi wenye sifa.
Shule za Kidato cha Tano na Sita zinatakiwa kuwa na mahitaji
ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano sahihi wa vyoo, bafu, vyumba vya
madarasa, bweni, jiko, bwalo, maktaba, maabara, chumba cha Jiografia; pamoja na
samani kulingana na idadi ya wanafunzi.
Shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne ambazo
zinahitaji kuanzisha kidato cha Tano, zinatakiwa kuwa na miundombinu na
mahitaji kamilifu yanayotosheleza kidato cha Kwanza hadi cha Nne kabla ya
kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita.
Natoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa wawaelekeze Wakurugenzi
wa Halmashauri, Miji na Majiji kuhakikisha azma ya Serikali ya kila Tarafa kuwa
na shule ya Kidato cha Tano inatekelezwa ili kupunguza idadi ya wanafunzi
wanaokosa nafasi. Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi
tunahimiza shule zitakazoanza Kidato cha Tano ziwe na maabara ili kuongeza
idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi.
Aidha, shule ambazo hazikupangiwa wanafunzi kutokana na
mapungufu mbalimbali, Makatibu Tawala wa Mikoa husika wanahimizwa kuwaelekeza
Wakurugenzi kusimamia kwa karibu ukamilishwaji wa shule hizo ili ziweze kupokea
wanafunzi wa chaguo la pili (Second selection).
Natumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa Elimu
kuhakikisha kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha Tano ziwe za
bweni kwa kuwa wanafunzi wa kutwa ni wachache na ni lazima watoke eneo husika.
Kwa mfano, mwaka huu shule ya sekondari Buswelu ya mjini Mwanza imekosa
wanafunzi kwa kuwa ni ya kutwa na Mwanza kuna shule 3 za kutwa. Hivyo ilikuwa
vigumu kupata wanafunzi wa eneo hilo wa kutosheleza shule hizo.
Wakuu wa Shule wahakikishe kuwa wanafunzi wa kidato cha nne
wote wanajaza ‘Selforms’ kwa umakini na kwa usahihi ili kurahisisha zoezi la
uchaguzi. Aidha, wazazi kwa kushirikiana na walimu wawaelekeze watoto wao kuwa
na dira, kuwasaidia kusoma kwa malengo na kufanya machaguo ya tahasusi
kulingana na dira walizonazo.
10.0 WANAFUNZI KURIPOTI KATIKA SHULE WALIZOPANGWA
Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano mwaka huu
2014,utaanza mwezi Julai tarehe 10. Wanafunzi wamepangwa katika shule zenye
miundombinu na walimu kwa masomo husika. Aidha, iwapo baadae mapungufu
yatajitokeza, wakuu wa shule wameelekezwa kutoa taarifa kwa uongozi wa
Halmashauri husika kuhusu upungufu huo.
Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano
umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa kuzingatia machaguo ya wanafunzi
pamoja na ufaulu hivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote.
Kwa nafasi hii, naagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule
walizopangwa tarehe 10 Julai, 2014. Wanafunzi ambao watashindwa kuripoti
shuleni hadi tarehe 30 Julai, 2014 nafasi zao zitajazwa na wanafunzi ambao
wamekosa nafasi.
Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2014, walimu,
wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa elimu kwa jitihada za
kuwaandaa wanafunzi, na kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano. Ushirikiano wa
wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini.
Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule wawe na utaratibu
endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo yanayopimika. Katika
utaratibu wa ”Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)”; kila mmoja anatakiwa
kuacha utendaji wa mazoea na afanye kazi kwa malengo na viwango, kuwa na
mipango inayotekelezeka ya muda mfupi na muda mrefu na kuwa na vipindi vya
tathmini kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji. Ni matumaini
yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu wakizingatia taratibu hizi,
elimu inayotolewa hapa nchini itaendelea kuwa bora zaidi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Mhe. Kassim M. Majaliwa (MB)
OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI
-------------------------------------------------
No comments:
Post a Comment