MSANII Emmanuel Mbasha (32) na mume wa Mwimbaji wa Injili,
Flora Mbasha, amefikishwa Mahakama ya
Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la ubakaji.
Mshtakiwa huyo ambaye ni mfanyabiashara na mwimbaji
alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Wilberforce Luago.
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga alidai kuwa mshtakiwa
alitenda makosa hayo mawili maeneo ya Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam.
Katuga alidai katika shitaka la kwanza kuwa, Mei 23, mwaka
huu eneo la Tabata Kimanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria huku akijua ni kosa
alimuingilia kwa nguvu msichana anayedaiwa kuwa shemeji yake (jina
limehifadhiwa).
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 25, mwaka huu eneo
la Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa
alimuingilia kwa nguvu mfanyakazi wake
(jina limehifadhiwa).
Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashitaka hayo .Upande wa
Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi la dhamana.
Hakimu Luago alitaja masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kuwa
na wadhamini wawili, mmoja awe mtumishi wa serikali na mwingine kutoka taasisi
inayotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 5.
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo
alipelekwa rumande na kesi iliahirishwa hadi Juni 19, mwaka huu itakapotajwa.
Mbasha akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi alisindikizwa
katika basi la Jeshi la Magereza kwa ajili ya kwenda kuanza maisha mapya
mahabusu ya Keko, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment