Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Jimbo la Monduli,
Edward Lowassa ametangaza kuanza kwa hatua za kuyarejesha kwenye Mamlaka za
Serikali za Vijiji mashamba 21 ya wawekezaji yenye ukubwa wa zaidi ya ekari
10,000, ambayo hayajaendelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lomooti, Kata ya
Lolkisale wilayani humo alipokwenda kutembelea boma la kisasa la mfugaji Isaya
Lembekure, Lowassa alisema haiwezekani wananchi wa Monduli kukosa ardhi wakati,
kuna ardhi yao iliyohodhiwa na wachache bila kuendelezwa.
“Monduli tumechoka na uuzwaji wa ardhi. Kila mahali
ni matatizo ya uuzwaji wa ardhi. Sasa tunatangaza kuanza mchakato wa kuyarejesha
mashamba yote ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa. Tayari hatua mbalimbali
zimeanza kuchukuliwa ili kuyarejesha,” alisema
Lowassa.
Tamko hilo la Lowassa, lilipokewa kwa shangwe na
wananchi wa Wilaya ya Monduli na limekuja wakati migogoro ya ardhi baina ya
wawekezaji na wananchi na wakulima na wafugaji imeshamiri
nchini.
Licha ya kutoa agizo hilo, Lowassa ameendelea kukemea
uuzajiwa wa ardhi wilayani humo, unaofanywa kinyume cha taratibu na
Serikali.
“Kuanzia sasa kiongozi wa kijiji atakayebainika
kuhusika kuuza ardhi kinyemela, ang’olewe kupitia mikutano ya vijiji,”
alisema Lowassa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Monduli, Twalib Mbasha alisema tayari halmashauri hiyo imeanza maandalizi ya
kuyarejesha mashamba hayo kwa kuwataka wahusika wa mashamba hayo kujieleza kwa
nini hawajayaendeleza hadi leo.
“Halmashauri inakusudia kuyafuta mashamba yote
yasiyoendelezwa na yaliyotelekezwa, hii ni kutokana na kushindwa kufuata
masharti ya ardhi kama ilivyoanishwa na sheria ya Ardhi namba 4,999 fungu la 44
na fungu la 48. Nimetoa siku 90 watu hawa wajieleze,” alisema
Mbasha.
Aliyataja mashamba yanayotarajiwa kurejeshwa kwenye
mamlaka za Serikali za Vijiji kuwa ni Meru Enterprises namba 10, ACU LTD namba
2390, TANFORM LTD 47, TANFORM 44 na Melembuki Kitesho Mollel namba 974 katika
Kijiji cha Lolkisale.
Mashamba mengine ni The Monduli Parents Sec School,
Musa Mamuya namba 2278 lipo Makuyuni, David Pello 2275, Hillary Gadi namba 2474,
Khalifan Said Masoud 2276, Masoud Said Masoud 2277 yapo Kijiji cha Mswakini
Juu.
Alitaja pia yaliyopo katika kijiji hicho ni ya Lucas
Petro Kambei namba 2597 na Rungwa game Safari Ltd namba
2765.
Alisema mashamba mengine ni Omary Daudi Mshana 1571,
Saidi Rashid Lena namba 2549 yaliyopo Kijiji cha Naitolia, wakati mashamba
mengine ni ya T.R Msuya namba 3, Esimingori Estate Ranch namba 7/2, Saburi
Estate Ltd namba 7, Musa Y. Mamuya yaliyopo Makuyuni.
No comments:
Post a Comment