Monday, June 23, 2014

Rais wa Malawi aoa kwa Shilingi Milioni 155

Baada ya miaka 30 ya kuishi bila ya ndoa, Rais mpya wa Malawi, Profesa Peter Mutharika, hatimaye amefunga pingu za maisha na mbunge wa zamani wa Jimbo la Balaka, Gertrude Maseko.
 
Kabla ya ndoa yao iliyofungwa jana kwenye Kanisa la Mtakatifu Michael na Malaika Wote jijini Blantyre, Maseko aliwahi kuolewa, lakini ndoa yake ilivunjika miaka kumi iliyopita; na mwaka jana mume wake huyo, ambaye pia alizaa naye mtoto mmoja, anayesoma Chuo Kikuu, aliaga dunia.
 
Aidha, kwa Rais Mutharika, Profesa aliyebobea katika masuala ya sheria, aliwahi kumwoa Christophine G. Mutharika, raia wa Visiwa vya Carribean. Alibahatika kuzaa naye watoto watatu, Mahopela ambaye ni wa kiume na mabinti, Monique na Moyenda, ambao wote ni wanasheria mahiri nchini Marekani kwa sasa.
 
Hata hivyo, Mutharika alimpoteza mkewe huyo kwa ugonjwa wa kansa mwaka 1990, hivyo kumfanya asioe kwa muda mrefu, huku akijikita zaidi katika kazi zake za uwakili kwa zaidi ya miaka 40 nchini Marekani.
Katika ndoa iliyoongozwa na Padri Rapson Chikwenzule, Rais Mutharika hakuwa na mbwembwe nyingi kama mkuu wa nchi na alitarajiwa kuendelea na sherehe katika shamba la familia ya Rais huyo lililopo Ndata Wilaya ya Thloyo, Kusini mwa Malawi.
 
Ukiondoa makundi ya marafiki na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi, miongoni mwa walioshuhudia wawili hao wakioana ni mabinti wa Mutharika, ambao walikanyaga ardhi ya Malawi kwa mara ya kwanza baada ya baba yao kuutwaa urais wa Malawi Juni Mosi, mwaka huu.
 
Kaka yao ambaye pia ni profesa katika moja ya vyuo vikuu vya Marekani, hakuhudhuria na hajawahi kukanyaga nchi ya Malawi.
 
Hata hivyo, ujio wa watoto hao umemaliza uvumi, uliokuwa umeenezwa wakati wa kampeni za urais, kwamba Mutharika si mwanamume aliyekamilika na hajawahi kuwa na watoto.
 
Akizungumza siku moja kabla ya harusi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Harusi ya Rais Mutharika na Maseko, Saulos Chilima ambaye ni Makamu wa Rais wa Malawi, alisema harusi ya `bosi’ wake ilitarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 95,000 (Sh milioni 155).
 
Alisisitiza kuwa fedha hizo si za Serikali, bali ni michango kutoka kwa pande mbili za maharusi, hasa ndugu na marafiki.
 
“Kila kitu kimekwenda sawa, nashukuru dhamira ya kutogusa fedha za Serikali imetimia. Michango imetoka kwa ndugu na marafiki. Kuna watu waliotaka kutumia mwanya wa harusi kujiweka karibu na Rais au wasaidizi wake, hawa ‘tuliwafungia vioo’. Hatukutaka baadaye waje kutusumbua wakitaka kusaidia kufanikisha mambo yao kwa kigezo cha ukaribu na Rais na hasa kwa kushiriki kikamilifu katika harusi yake. Hilo tumesema hapana, hatutaki rushwa na tutapambana kwa dhati na rushwa na wala rushwa,” alisema Chilima.
 
Mutharika (74) ambaye ni Rais wa Tano wa Malawi, anakuwa Rais wa tatu kuoa akiwa madarakani. Wa kwanza kuoa akiwa Ikulu, alikuwa Bakili Muluzi ambaye baada ya kuachana na Anne, alimwoa Shanil Dzimbili.
 
Baadaye, Bingu wa Mutharika, Rais wa Tatu ambaye ni kaka wa Rais wa sasa, yeye alimwoa Callista Mutharika baada ya kufiwa na mkewe, Ethel.
 

Marais wengine waliowahi kuitawala Malawi ni Dk Hastings Kamuzu Banda ambaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Malawi na Joyce Banda, Rais wa Nne ambaye ameangushwa na Profesa Mutharika katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 20, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment