Hakuna neno zuri la
kusema zaidi ya Mungu mkubwa. Ule mtafaruku ndani ya ndoa ya mwimba Injili
mahiri Bongo, Flora na mumewe, Emmanuel Mbasha umedaiwa kumalizika kwa wawili
hao kupatana.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, wawili hao walikalishwa kikao
cha upatanishi mapema wiki hii kilichokuwa chini ya familia.
MANENO YA CHANZO
“Kikao cha familia kilikaa, Mbasha aliitwa akafika, Flora naye
aliitwa akatokea, mazungumzo yalikuwa marefu lakini kimsingi waliamua kuweka
kando mtafaruku wao na kuijenga upya ndoa yao,” kilisema chanzo.
Chanzo kiliongeza kuwa katika kikao hicho cha mwanzoni mwa wiki
hii, miongoni mwa adidu za rejea ilikuwa kutokumbushia vikao vilivyopita ambapo
hakukupatikana muafaka.
VIKAO VILIVYOPITA
Katika vikao vilivyopita, wahusika wakuu walikuwa wazazi wa
Mbasha (mzee Maneno Mbasha, Zulfa Maneno), ndugu wa Flora na Mchungaji wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
VIKAO VYA BAADAYE
Kwa mujibu wa chanzo, vikao vilivyofuata, wawili hao wakawa
tayari kila mmoja ametema nyongo yake pembeni na kufikia makubaliano kwamba,
ndoa yao isimame tena wakitumia maandiko kwenye Biblia kutoka kitabu cha
Waebrania yanayosema: Ndoa na
iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi
Mungu atawahukumia adhabu.
WAKORINTHO YAFUNGA KAZI
Kwa mujibu wa chanzo hicho, maneno mengine ya Biblia
yaliyotumika kwenye kikao hicho mpaka wawili hao wakaamua kurudiana ni 1
Wakorintho 7:1-10 ambapo maandiko yanasema:
Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake
mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki
yake vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe vivyo hivyo mume
hana amri juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmepatana kwa
muda ili mpate faragha kwa kusali, mkajiane tena shetani asije akawajaribu kwa
kutokuwa na kiasi kwenu.
Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza, wala hapo si mimi, ila
Bwana (Mungu), mke asiachane na mumewe, lakini ikiwa ameachana naye na akae
asiolewe au apatane na mumewe, tena mume asimwache mkewe.
KIKAO CHA JUMAMOSI KUMALIZIA
Chanzo kilisema kuwa, kikao cha mwisho ambacho kitamalizia
kuweka mambo sawa ili wawili hao waanze ngwe ya pili ya ndoa yao ambayo
inaaminika itakuwa ya mwisho mpaka kifo kiwatenganishe, kinatarajiwa kufanyika
leo jijini Dar es Salaam mahali ambapo hapakutajwa.
MWANASHERIA ATAJWA
Mwanasheria wa Flora aliyejulikana kwa jina moja la Ado ametajwa
kusimamia kikao hicho ili wawili hao waanze maisha mapya baada ya safari fupi
ya mvurugano uliowafanya kuwa mbalimbali.
Juzi, Risasi Jumamosi lilimsaka mwanasheria huyo kwa njia ya
simu yake ya mkononi ili kumsikia anasemaje kuhusu kutajwa kwenye usuluhishi wa
ndoa hiyo ambapo alipopatikana alisema:
“Niko Arusha, Ijumaa nitarudi Dar. Kuhusu kikao cha usuluhishi
siwezi kukwambia lakini suala la kuwapatanisha nalifahamu, nawaomba na ninyi
msaidie kufanikisha jambo hilo zuri.”
VIPI KUHUSU KESI YA MADAI YA KUBAKA?
Hata hivyo, Wakili Ado hakutaka kugusia kuhusu kesi ya Mbasha
iliyopo Mahakama ya Wilaya ya Ilala ambapo anadaiwa kumbaka shemejiye mara
mbili (jina tunalo) ambayo kwa mujibu wa mahakama, upelelezi umekamilika na
itasikilizwa Julai 17, mwaka huu.
KWA UPANDE WAKE FLORA
Risasi Jumamosi lilimwendea hewani, Flora ili kumsikia anasemaje
kuhusu kuwepo kwa upatanishi kati yake na mumewe, Emmanuel.
Huyu hapa: “Ongea na wakili wangu atakwambia kila kitu.” Ambapo
majibu ya wakili yalikuwa: ”Ninachojua mimi ni kwamba Flora ameshamsamehe
mumewe na yuko tayari kuanza ukurasa mpya.”
MBASHA SASA
Kwa upande wake, Mbasha alipozungumza na Risasi juzi alisema
kurejea upya kwa ndoa yake ni jambo la kuupendeza moyo wake.
“Mimi sina neno nipo tayari, nimeshasamehe yaliyotokea, Flora ni
mke wangu jamani, nampenda sana kutoka moyoni.”
Chanzo: Risasi jumamosi
/Gpl
No comments:
Post a Comment