Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana sifa za kugombea tena uongozi wa chama
hicho kwa kuwa wanabanwa na katiba yao.
Akizungumza jana ofisini kwake baada ya kuzungumza na
Mbowe, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza alisema walipata malalamiko na
kuyafanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kupitia kumbukumbu walizonazo na kubaini
kuwa kipengele cha ukomo wa uongozi kiliondolewa kinyemela katika katiba ya
chama hicho.
Alisema kwa kawaida vyama vyote vinapofanya mikutano
huwapelekea muhtasari, hivyo Chadema nacho kiliwapelekea kumbukumbu ya Mkutano
Mkuu wa mwaka 2006, lakini hakuna sehemu yoyote iliyoondoa ukomo wa uongozi.
“Hivyo, hawa tayari wana vipindi viwili, wakichaguliwa
katika uchaguzi unaokuja hatutawatambua. Wakitaka wabadili katiba kwa njia
halali ambayo ni ya mkutano mkuu na si vinginevyo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mbowe alisema hakuwa tayari
kulizungumzia, akieleza kwamba amefika kwenye ofisi hiyo ya Msajili kwa masuala
mengine.
“ Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa, likifikishwa
kwenye Kamati Kuu ndipo nitalielezea,” alisema Mbowe.
Baadaye Ofisa wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema
kwamba Msajili alimwita Mbowe ili kumshawishi asaidie wajumbe wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) warejee katika Bunge la Katiba.
“Mwenyekiti alibainisha kuwa msimamo wa Ukawa upo wazi
kwamba hawatarudi katika Bunge hilo hadi pale maoni ya wananchi yatakapoanza
kujadiliwa na msimamo huo hautabadilika,” alisema Makene akimkariri Mbowe.
Makene alisema baada ya kutoa msimamo huo, hakuna maongezi
mengine yaliyoendelea baina ya Mbowe na Msajili.
Alipoulizwa iwapo Msajili alionyesha nia pia ya
kuushawishi upande wa pili wanaotaka serikali mbili, Makene alisema hawezi
kufahamu, japo kwa nafasi yake, Mutungi ana uwezo wa kufanya hivyo.
Alipoulizwa iwapo Msajili pia alizungumzia suala la ukomo
wa uongozi linalodaiwa kubadilishwa kinyemela, alisema: “Kuhusu hilo Chadema
tunafuatilia kwa kina taarifa zinazozagaa zikionyesha correspondence (barua)
zinazotoka kwa Msajili wa Vyama juu ya Chadema na tutakapokamilisha tutatoa
taarifa.”
Mpekuzi jana ilichapisha
taarifa iliyonukuu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, ikieleza kuwa kipengele hicho katika Ibara
ya 6.3.2 (C) kiliondolewa kwenye katiba bila idhini ya mkutano mkuu wa chama
hicho.
Jaji Mutungi alisisitiza kuwa mkutano mkuu wa chama hicho
ndiyo wenye mamlaka ya kurekebisha katiba, hivyo baada ya kupitia muhtasari wa
Mkutano Mkuu wa mwaka 2006 suala la kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi
halikuonyesha kujadiliwa katika mkutano huo.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu juzi, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kipengele hicho kiliondolewa kwa vikao vya
chama ambavyo ni wilaya na mkoa.
Hoja hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na ambaye sasa si mwanachama wa chama hicho.
Source: Mpekuzi.
No comments:
Post a Comment