Tuesday, July 1, 2014

Mwanamke Auawa kikatili na mpenzi wake kisa Wivu wa Mapenzi

Mkazi wa Mtaa  wa Majengo ‘B’ mjini Mpanda, Cesilia Clement (22) ameuawa kikatili  kwa  kuchomwa kisu mwilini na mpenzi wake, aliyemtuhumu kutomjali  baada ya kuwa na  mahusiano  ya kimapenzi  na mwanamume mwingine.
 
Mtuhumiwa aliyefahamika kwa jina moja la Kanu, ambaye ni mkazi wa Kigoma naye amejijeruhi vibaya kwa kujikata koromeo, alipojaribu kujichinja  baada ya kubaini  kuwa  amemuua  mpenzi  wake Cecilia. Pia, mtu huyo anadaiwa  kujichoma  kisu  tumboni.
 
Taarifa kutoka  eneo  la  tukio  na zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa  wa Katavi, Dhahiri  Kidavashari  zinaeleza kuwa  mtuhumiwa huyo ni mfanyabiashara wa mpunga.
 
Taarifa hizo zilisema mtu huyo anatuhumiwa kutenda  uhalifu huo  saa  mbili  asubuhi  nyumbani  kwa shemeji wa marehemu,  aitwaye Mashaka Hanja katika Mtaa wa Majengo “B” mjini hapa.
 
Ilidaiwa kuwa katika uhai  wake,  Cesilia alikuwa  akiishi kwa dada yake, ambaye ni  mke wa Mashaka Hanja na alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Kanu, ambaye alikuwa amepanga  katika  nyumba hiyo.
 
Mashuhuda  na majirani  wa Mashaka, walidai kuwa siku  hiyo  ya tukio, Cesilia aliamka saa mbili asubuhi na kuanza kufagia  uwanja wa  nyumba  hiyo  ya shemeji yake Mashaka.
 
Inadaiwa kuwa wakati Cecilia akiendelea kufanya usafi katika  nyumba hiyo,   Kanu alitoka  nje  ya chumba alichopanga  katika nyumba hiyo na  kumwita  Cesilia, kisha wote  wakaingia ndani  ya chumba  chake.
 
“Tulimsikia  Kanu  akimwita  Cecilia,  kisha tukawaona  wote  wakingia katika  chumba alichopanga  Kanu,  ndipo  ghafla  tukasikia  Kanu  akifoka kwa sauti kubwa, akimshutumu  Cesilia kuwa siku  hizi  amekuwa hamjali kabisa,  kwa kuwa  ana mahusiano  na mwanamume mwingine “  alidai  mtoa taarifa.
 
Inadaiwa    baada ya mabishano ya muda mfupi, wapangaji  na  majirani walisikia  Cesilia akipiga mayowe  ya kuomba msaada. Lakini, jitihada zao  za  kuufungua mlango  wa chumba hicho  cha Kanu, zilishindwa kwani ulikuwa umefungwa kwa ndani.
 
“Tulijaribu  kumsihi   Kanu afungue mlango, lakini alikaidi  ndipo tukalazimika  kuchungulia  dirishani  na  kushuhudia  jinsi Kanu akimshambulia  Cecilia  kwa kisu, akimchoma  sehemu mbalimbali  za mwili wake ....huku Kanu  akiwa ametapakaa  damu  mwili  mzima “ anadai mmoja wa mashuhuda.
 
Kwa mujibu  wa Kamanda Kidavashari, askari  Polisi  walifika  eneo  hilo la tukio,  baada ya kutaarifiwa. Alisema polisi walikuwa na silaha,  ambapo  walivunja mlango wa chumba  hicho  cha Kanu na  kuushuhudia mwili  wa marehemu  ukiwa  umelala  kwenye dimbwi  la  damu  sakafuni,  akiwa tayari mfu.
 
Ilidaiwa kuwa  Kanu  naye alikuwa amezirai,  baada ya kujijeruhi vibaya shingoni  na tumboni  kwa  kisu, baada ya kubaini kuwa amemuua mpenzi wake.
 
Kwa sasa Kanu amelazwa  katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, mjini hapa,  kwa matibabu  akiwa chini ya ulinzi mkali.
 
Kamanda Kidavashari alidai kuwa mtuhumiwa  huyo,  atafikishwa mahakamani baada ya kutibiwa na kupona. Uchunguzi  wa tukio  hilo  bado unaendelea.
 

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ili ufanyiwe uchunguzi  wa kitabibu,  kabla ya  kukabidhiwa  ndugu wa marehemu kwa maandalizi ya maziko yake.

Source:Mpekuzi.

No comments:

Post a Comment