David Kafulila |
Vigogo wa IPTL na PAN AFRICAN |
Kesi hiyo ya madai namba 131 ilifunguliwa wiki iliyopita Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupitia wakili wa kujitegemea Augustine Kusalika.
Walalamikaji hao wanaiomba mahakama imwamuru Kafulila kuwalipa fidia ya Sh. bilioni 310 kwa madai ya kutoa kashfa dhidi yao ya kuwatuhumu kujipatia pesa kutoka katika akaunti ya Escrow, kwa njia zisizo halali.
Katika hati ya madai, ilidaiwa kuwa kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Bunge, Kafulila anadaiwa kuwatuhumu PAP na Seth kuchota Sh. bilioni 200 kutoka katika akaunti hiyo kupitia IPTL isivyo halali, huku akiwataja mawaziri na maofisa wengine wa serikali kuhusika katika wizi huo.
Hati hiyo iliendelea kudai kuwa walalamikaji wanaiomba mahakama imwamuru Kafulila awalipe Sh. bilioni 210 kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi zao.
Pia wanaiomba mahakama imwamuru mdaiwa awalipe Sh. bilioni 100 kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana na taarifa za kashfa zilizotolewa na mdaiwa dhidi yao.
Mbali na fidia hizo, pia walalamikaji wanaiomba mahakama imwamuru mdaiwa awaombe radhi kutokana na taarifa hizo za kashfa, ambazo wanadai zimewashushia hadhi.
Maombi mengine ni gharama za kesi, riba kwa kiasi cha pesa yote wanayodai kwa kiwango cha asilimia cha mahakama, kutoka tarehe ya hukumu hadi tarehe ya mwisho wa malipo hayo na amri nyinginezo, ambazo mahakama itaona zinafaa.
Aidha, hati hiyo ya madai inaeleza kuwa mlalamikaji wa kwanza amekuwa akitekeleza mkataba baina yake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akilisambazia umeme Tanesco na pamoja na kutekeleza wajibu wake kama ilivyo katika makubaliano ya mkataba.
Kadhalika, inabainisha kuwa mlalamikaji wa kwanza amekuwa na mgogoro na Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited pamoja na Tanesco.
Inaeleza kuwa kutokana na mgogoro huo kiasi cha Sh. bilioni 200 ziliwekwa katika akaunti ya Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa ajili ya kusubiri kumalizika kwa mgogoro huo uliokuwa mahakamani hapo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa mgogoro huo ulimalizika na kuhitimishwa kwa mdai wa kwanza (IPTL) kupata amri ya mahakama kumiliki pesa hizo zilizokuwa katika akaunti hiyo na pia BoT ikitakiwa kuziachia.
Hati hiyo inaeleza kuwa katika hali ya kushangaza na pasipo na uhalali wowote, mdaiwa katika matukio tofauti na nje ya Bunge aliamua kusambaza kwenye mitandao ya kijamii taarifa za kashfa dhidi ya mdai wa kwanza na mdai wa tatu.
Mitandao hiyo ya kijamii ni ya Jamii forum, Twitter na Facebook, ambayo kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, mdaiwa amekuwa akiitumia kusambaza taarifa hizo za kashfa dhidi yao.
Hati hiyo pia inaeleza kuwa Juni, 2014, mdaiwa alichapisha kuwa mdai wa kwanza na wa tatu walijipatia pesa kutoka akaunti ya Escrow isivyo halali, wakati si kweli. “Bila uhalali wowote, mdaiwa alisambaza taarifa kuwa mdai wa kwanza amehusika katika vitendo viovu vya kuchukua pesa hizo katika akaunti ya Escrow, jambo ambalo si kweli,” inasomeka hati hiyo.
Pia ineeleza kuwa mdaiwa amekuwa akitoa taarifa za kashfa, huku akimuita mdai wa tatu kuwa ni Singasinga, jambo ambalo si sawa na linaharibu sifa yake na kusababisha uendeshaji wa biashara zake zinazofanywa na mdai wa kwanza na wa pili kudorora.
Hati hiyo ya madai inaeleza kuwa kitendo cha mdaiwa kutoa taarifa hizo za kashfa kimesababisha jamii kwa jumla kuamini kuwa mdai wa kwanza amejipatia pesa hizo kutoka katika akaunti hiyo isivyo halali na kwamba, raslimali zao zinahujumiwa na mdai wa kwanza.
“Kitendo cha mdaiwa kutangaza kwa jamii taarifa za mdai wa kwanza kujihusisha na mchezo mchafu, kimesababisha hasara au kupungua kwa hadhi ya mdai wa kwanza na wa pili” inaeleza hati hiyo ya madai.
Inaongeza kuwa mdaiwa akiwa ni mbunge ana kinga ya kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa yale aliyoyasema bungeni, lakini pia inabainisha kuwa taarifa hizo za kashfa zimesambazwa na mdaiwa nje ya Bunge.
Hati hiyo ya madai inasisitiza kuwa kitendo cha mdaiwa kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwa jamii si tu kwamba, kimeshusha hadhi ya mdai, bali pia kimesababisha hasara ya kibiashara.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, mdaiwa bado anaendelea kutangaza taarifa hizo za kashfa dhidi ya wadai, licha ya taarifa ya maneno na ya maandishi aliyopewa, hivyo kusababisha hadhi ya wadai kuendelea kushuka na kusababisha hasara kibiashara.
Hati hiyo inadai kuwa hadhi yao si tu kwamba, imeshuka ndani ya nchi pekee, bali pia kimataifa na hivyo kuwasababishia hasara kibiashara, na kwamba, taarifa hizo pia zimewasababishia madhara ya kisaikolojia na usumbufu kwa menejimenti nzima.
Inaeleza kuwa kitendo cha mdaiwa kuelezea mambo yaliyojiri katika mahakama za kisheria katika maombi baina ya mdai wa kwanza na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, kimesababisha si tu kuingilia uhuru wa mahakama, bali pia hasara kwa mdai wa kwanza.
Wadai wanaendelea kueleza kuwa mdaiwa alikuwa akijua kilichoendelea mahakamani katika maombi hayo baina ya mdaiwa wa kwanza na VIP, lakini aliamua kutangaza kinyume kuhusu akaunti ya Escrow.
Hati hiyo inasisitiza kuwa mdai wa kwanza alipata pesa hizo kutokana na amri halali ya mahakama baada ya uamuzi wa maombi hayo baina yake (IPTL) na VIP.
Kadhalika, inadai kuwa kwa kuwa mdaiwa wa kwanza anatoa huduma ya kulisambazia Tanesco umeme, taarifa hizo za mdaiwa zimehatarisha uhusiano baina yake (mdai) na Tanesco na hivyo kusababisha kudorora kwa uchumi na biashara ya wadai.
KAFULILA: SINA WASIWASI
Kwa upande wake, Kafulila akizungumza na NIPASHE alisema kwa sasa yuko mkoani Kigoma kueleza wananchi juu ya madai yake ya kuwapo kwa ufisadi anaodai kuwa ulifanyika katika akaunti ya Escrow na kwamba, alichokisema ni kweli na hana wasiwasi.
“Hivi ninavyozungumza niko mkoani Kigoma kueleza wananchi juu ya ufisadi huo. Sina wasiwasi. Watangulie tu mahakamani na ninaamini nilichokisema ni ukweli,” alisema Kafulila.
Source: Nipashe
No comments:
Post a Comment