Monday, July 7, 2014

Sabasaba 2014 kuunganisha Uzalishaji na Masoko

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, TANTRADE Bibi Jaqueline Mneney Maleko akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu Maonyesho ya 38 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara ya Nje wa TANTRADE, Bibi. Anna Bulondo.

-Kiingilio ni kama mwaka jana, Banda maalumu kuitangaza Tanzania
 -Nchi 31 kushishiriki, zipo pia Wizara na Taasisi za Serikali, Mashirika na Makapuni binafsi.

Na Johary Kachwamba- MAELEZO
Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar-es-salaam (38th DITF) yanatarajia kuanza tarehe  28 mwezi huu na kufikia kilele chake tarehe 8 Julai  2014 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya kilwa, jijini Dar-es-salaam.

Akitoa taarifa hiyo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bibi. Jacqueline Mneney Maleko imeeleza kuwa maonesho  ya  mwaka huu yataongozwa na kauli mbiu isemayo “Tunaunganisha Uzalishaji na Masoko”

Amesema kuwa Kauli Mbiu hiyo imechaguliwa kutumika kuonesha uhusiano uliopo kati ya Uzalishaji na Masoko  na umuhimu wa mnyororo wa uzalishaji ambao ndio chimbuko la upatikanaji wa Bidhaa bora zenye ushindani katika soko.

Bibi. Maleko amesema kuwa mwaka huu TanTrade imetenga eneo kubwa zaidi kwa ajili ya Wazalishaji wa ndani ya nchi na kubainisha maeneo yatakayotumiwa na wazalishaji hao kuwa ni jengo namba C.19 na eneo la wazi lililo nyuma ya ofisi za Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Uwezeshaji kwa ajili ya bidhaa za kilimo na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.

Kuhusu ushiriki wa mataifa mengine katika maonesho hayo amefafanua kuwa tayari nchi 31 zimethibitisha kushiriki maonesho hayo zikiwemo Afrika Kusini,Czech Republic, China, Ghana, Indonesia, India, Iran, Finland, Ugiriki, Italia, Japan, Jordan, Kenya, Korea ya Kusini, Malaysia, Marekani, Misri, na Ujerumani.

Nchi zingine ni pamoja na Nigeria, Pakstani, Rwanda, Saudi Arabia, Singapore, Sudani, Syria, Uganda, Uingereza, Burundi, Sweden, Vietnam na Zimbabwe.

Aidha, amefafanua kuwa makampuni ya nje 490 yamethibitisha kushiriki katika maonesho hayo huku  Wizara na Taasisi za Serikali zilizothibitisha kushiriki maonesho hayo zikifikia 61.

Kwa upande wa Mikoa amesema tayari mikoa 10 imethibitisha kushiriki ikiwemo, Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mara, Manyara na Ruvuma. Jumla ya Washiriki waliothibitisha kushiriki kutoka ndani ya nchi ni 1700.

Kuhusu  kiingilio wakati wa maonesho hayo amesema watu wazima walipia  Shilingi 2,500 na watoto ni 500 kila siku kwa siku zote za maonesho isipokuwa tarehe 7 Julai,2014 ambapo ada itakuwa Shs. 3,000/= kwa watu wazima  na watoto ni Shs.1000/=

No comments:

Post a Comment